Friday, 1 November 2013

Maisha

Ndugu zangu, hakuna kitu ambacho
kimekuwa kikiniumiza kama kuona watu
wanakoseana kisha wanawekeana
vinyongo. Kukerwa kwa jambo hilo
ndiko kulikonifanya niandike mada hii
nikiamini itawabadili wale ambao
wanaona kuomba msamaha au
kusamehe ni jambo gumu kwao.
Kiukweli utu wa mtu huweza
kuthibitishwa kwa vitu vidogo sana.
Binadamu hatuko kamili kwani
tumepewa udhaifu ikiwa ni pamoja na
kuwa wakosaji. Lakini licha ya kuwa na
udhaifu huo pia tumepewa nafasi ya
kuomba msamaha pindi tunapojikuta
tumekosea.
Ni kutokana na udhaifu huo tulionao
ndiyo maana wakati mwingine
tunajikuta tunafanya ama kusema
mambo ambayo yanawaumiza wengine
na hakuna njia mbadala ya kuondoa
maumivu hayo zaidi kuomba msamaha
kwa wale ambao tumewaumiza.
Sikatai ukweli uliopo kwamba kwa
kuomba msamaha tu hakuwezi
kupunguza maumivu ambayo ameyapata
uliyemtendea lakini kidogo kwa
kuonesha utu na heshima uliyonayo
kwake na kulitamka kwa dhati kabisa
linaweza kupunguza athari kwake.
Unapoomba msamaha kwanza unajenga
mazingira ya amani na usawa.
Tumeshashuhudia watu wengi
wakigombana kutokana na kukosekana
kwa neno samahani. Unamkanyaga mtu
kwa bahati mbaya halafu unaona sawa!
Kuna utu kweli hapo? Utu hauwezi
kuwepo na matokeo yake unaweza
kusababisha ugomvi usiokuwa
w a lazima.
Ni dhahiri kwamba kama utamkosea
mtu halafu ukamuomba samahani, hata
kama alikuwa na lengo la kulipiza kisasi,
anaweza kutofanya hivyo kwani ataona
umeona kwamba ana haki ya kuombwa
samahani kutokana na kosa
alilotendewa.
Aidha, wanaofuata mafundisho ya
Mungu ni wale walioiva kiroho.
Unapofanya kosa halafu ukaomba
msamaha itaonesha ni jinsi gani
ulivyokua kiroho. Ni wachache sana
wanaothamini utu wa mtu. Mtu anaweza
kufanya kosa halafu akaona ni sawa tu
kumfanyia mwenzake vile bila kujua
kwamba amesababisha maumivu.
Kama ulikuwa hujui, samahani mara
nyingi inakuwa kama zawadi kwa
wakosewa, hii ni kwa kuwaonesha
wanastahili kuombwa msamaha na
kuonesha kwamba unamheshimu kwani
wengine hufikia hatua ya kuwashushia
hadhi waliowakosea na kuwaona si
lolote.
Siyo hivyo tu, samahani pia inaweza
kunusuru kuvunjika kwa uhusiano
uliopo baina ya watu wawili ama kikundi
na kikundi. Mara nyingi sana uhusiano
huvunjika kama kutatokea kukoseana
baina ya wawili. Lakini kama mmoja
atajitutumua na kuomba msamaha, ni
dhahiri uhusiano unaweza kuendelea
kuwepo. Mifano mizuri ipo kwa
wanandoa.
Wanandoa wangapi hukoseana lakini
suluhisho la yote linakuwa kuombana
msamaha? Wanandoa wanaokoseana
halafu wakatengana lazima atakuwepo
mmoja kati yao ambaye ni mgumu
kuomba msamaha ama atakuwepo
mgumu wa kusamehe. Tumeshuhudia
wengine wakifikia hatua ya kuomba
msamaha huku wakitoa machozi
kuonesha kwamba kweli wanakubali
kufanya kosa na wanajutia na
wanaomba msamaha na kuahidi
kutorudia tena.
Huo ndiyo msamaha ambao unaweza
kuzaa matunda. Unapofanya kosa halafu
ukaomba msamaha na kuonesha
kwamba hauko siriasi katika kufanya
hivyo basi fahamu kusamehewa ni
vigumu na kama itatokea kusamehewa
itakuwa kwa shingo upande na
mkosewaji anaweza kubaki na kinyongo
hali ambayo siyo nzuri kwa walio katika
uhusiano.
Tufahamu kwamba unapogundua
umefanya kosa na ukaomba msamaha,
unajitengenezea mazingira ya kugundua
udhaifu wako na kujua jinsi ya
kujirekebisha.
Unapofanya kosa halafu ukaona
kwamba hukufanya, ni vigumu sana
kujirekebisha na unaweza kujikuta kila
siku ni mkosaji kwa sababu unakuwa
mgumu wa kuyakubali makosa yako
kiasi cha kuweza kukufanya kila mtu
awe adui yako. Kubali makosa yako,
omba msamaha pale inapobidi ili
utengeneze mazingira ya amani.

No comments:

Post a Comment